Wakulima wa pamba kutoka kaunti ya Lamu wameitaka serikali kuimarisha sekta ya pamba kupitia mpango wa “Buy Kenya Build Kenya” kwa lengo la kuongeza uzalishaji, kupanua viwanda vya ndani vya nguo na kuinua hali ya uchumi wa wakulima pamoja na taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla ya uhamasisho kuhusu kilimo cha pamba iliyoandaliwa na Mamlaka ya Kilimo na Chakula (Agriculture and Food Authority, AFA), mkulima wa pamba kutoka eneo la Mpeketoni, Mary Mwangi, alisema kuwa wakulima bado wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo bei duni ya zao hilo na ukosefu wa masoko ya uhakika, hali inayowakatisha tamaa baadhi ya wakulima kuendelea na kilimo hicho.
Alisema kuwa endapo serikali itawekeza zaidi katika ujenzi wa viwanda vya kusindika na kutengeneza bidhaa za pamba nchini, wakulima watanufaika moja kwa moja kupitia soko la uhakika la mazao yao, sambamba na vijana wengi kupata nafasi za ajira katika sekta ya viwanda vya nguo.
“Serikali inapaswa kujenga viwanda vingi vya kutengeneza nguo za pamba nchini ili kuongeza nafasi za ajira kwa vijana na pia kuhakikisha pamba yetu inapata soko la ndani la uhakika,” amesema Mary Mwangi.
Kauli hiyo imeungwa mkono na mwenyekiti wa Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA), Cornelly Serem, pamoja na afisa mkuu wa kiwanda cha nguo cha Thika Cloth Mills, Tejal Dhodhia, ambao wamesema kuwa sekta ya pamba ina uwezo mkubwa wa kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa endapo itaungwa mkono ipasavyo na serikali.
Wamesema kuwa kwa sasa Kenya inaendelea kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuagiza nguo kutoka mataifa ya nje, hali ambayo inasababisha upotevu wa mapato na fursa za ajira ambazo zingeweza kuundwa ndani ya nchi kupitia viwanda vya ndani.
Aidha, wamesisitiza kuwa mpango wa “Buy Kenya Build Kenya” ni muhimu katika kuimarisha uzalishaji wa ndani, kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje na kuongeza mzunguko wa fedha ndani ya uchumi wa taifa.
NA HARRISON KAZUNGU.