Polisi katika eneo la Bondo, kaunti ya Siaya, wamemkamata mshukiwa mkuu anayehusishwa na mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST), tukio ambalo limewaacha wakaazi pamoja na wanafunzi wa chuo hicho katika hali ya huzuni na taharuki.
Mshukiwa huyo ametambuliwa kama Maximilian John Madeni, raia wa Tanzania ambaye anaripotiwa kuwa mfanyabiashara wa dhahabu. Polisi wanaamini kuwa mshukiwa huyo ana taarifa muhimu zinazoweza kusaidia kufanikisha uchunguzi kuhusu mauaji ya Alice Rianga mwenye umri wa miaka 20.
Mwili wa mwanafunzi huyo umepatikana katika eneo la Barkowino mjini Bondo baada ya wanawake waliokuwa wakikusanya kuni kugundua mwili ukiwa umetupwa kichakani na kutoa taarifa kwa maafisa wa polisi. Tukio hilo limewashtua wakaazi wa eneo hilo huku wengi wakitaka haki itendeke kwa familia ya marehemu.
Akizungumza na wanahabari, Kamanda wa Polisi wa Bondo Robert Aboki amesema kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa huenda marehemu ameuawa katika eneo tofauti kabla ya mwili wake kusafirishwa na kutupwa katika kichaka hicho.
“Tunaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hili. Ushahidi wa awali unaonyesha kuwa mwili huo umetupwa eneo la Barkowino baada ya mauaji kutekelezwa sehemu nyingine,” amesema Aboki.
Aidha, mwili wa mwanafunzi huyo umepatikana ukiwa hauna nguo za ndani jambo ambalo limeongeza mashaka kuwa huenda kumekuwa na uhalifu mwingine kabla ya mauaji hayo kutekelezwa.
Ripoti za awali zinaeleza kuwa Alice Rianga ametoweka tangu Jumatano iliyopita baada ya kuondoka katika hosteli yake kuelekea chuoni kwa shughuli za masomo lakini hakurejea. Familia, marafiki pamoja na wanafunzi wenzake wamekuwa wakimtafuta bila mafanikio hadi mwili wake ulipopatikana siku chache baadaye.
Mmoja wa wakaazi wa eneo la Barkowino amesema tukio hilo limewaogopesha wananchi wengi kutokana na namna mwili ulivyopatikana.
“Ni tukio la kusikitisha sana. Hatujawahi kushuhudia jambo kama hili katika eneo letu kwa muda mrefu,” amesema mmoja wa wakaazi.
Maafisa wa upelelezi wameanza kukusanya ushahidi pamoja na kuwahoji mashahidi mbalimbali ili kubaini mazingira kamili yaliyopelekea kifo hicho. Polisi pia hawajaondoa uwezekano wa kuwakamata washukiwa wengine kadri uchunguzi unavyoendelea.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ndogo ya Bondo ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa maiti ili kubaini chanzo halisi cha kifo chake huku familia ikiendelea kusubiri majibu kuhusu tukio hilo la kusikitisha.
Wakazi wa eneo hilo pamoja na viongozi mbalimbali wamewataka maafisa wa usalama kuhakikisha haki inapatikana haraka na waliohusika na mauaji hayo wanachukuliwa hatua kali za kisheria.
NA HARRISON KAZUNGU.