Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC Erastus Ethekon amesema kila chama cha kisiasa au mgombea anayeshiriki uchaguzi anaruhusiwa kuwa na wakala mmoja pekee katika kila kituo cha kupigia kura na wakala mkuu mmoja katika kituo cha kujumlisha kura.
“Kila chama cha kisiasa au mgombea anayeshiriki uchaguzi anaruhusiwa kuwa na wakala mmoja pekee katika kila kituo cha kupigia kura na wakala mkuu mmoja katika kituo cha kujumlisha kura. Hakuna kifungu cha sheria kinachoruhusu uwepo wa watu wasiokuwa na idhini rasmi kufanya shughuli ndani ya vituo vya kupigia kura au vya kuhesabia kura,” amesema Erastus Ethekon.
Ethekon ameongeza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa uwazi, amani na kwa mujibu wa sheria zilizowekwa, akisisitiza kuwa ni lazima watu wote wanaoruhusiwa ndani ya vituo vya kupigia kura wawe na kibali rasmi kinachotambulika na tume.
Aidha, ameeleza kuwa uwepo wa watu wasio na vibali rasmi ndani ya vituo vya kupigia kura au vya kujumlisha kura unaweza kuhatarisha ufanisi na uadilifu wa mchakato mzima wa uchaguzi.
Katika tahadhari nyingine, mwenyekiti huyo wa IEBC amewaonya wapiga kura dhidi ya kupiga picha karatasi za kura zilizowekwa alama, akisema kitendo hicho ni kosa la uchaguzi linaloweza kuadhibiwa kwa faini ya hadi shilingi milioni moja au kifungo cha miaka mitatu jela au adhabu zote mbili.

Amesema sheria za uchaguzi ziko wazi kuhusu faragha ya kura, hivyo ni muhimu kwa wapiga kura kuheshimu taratibu zilizowekwa ili kulinda uaminifu wa matokeo ya uchaguzi.
Matamshi hayo yanajiri huku wakazi wa eneo bunge la Emurua Dikirr wakijiandaa kushiriki uchaguzi mdogo leo kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Johana Ngeno aliyefariki baada ya ajali ya helikopta.
NA HARRISON KAZUNGU.