ALI MENZA MBOGO AISHAMBULIA SERIKALI YA NASSIR KWA KUTELEKEZA BILIONI 17 ZA MAENDELEO, AUNGWA MKONO NA VIONGOZI WA KIDINI.
By Dayo Radio
Published on 18/12/2025 19:46
News

Aliyekuwa mbunge wa Kisauni na mwenyekiti wa bodi ya Mradi wa LAPSSET, Ali Menza Mbogo, ameikosoa vikali serikali ya kaunti ya Mombasa inayoongozwa na Gavana Abdulswamad Sharif Nassir kwa kile alichokitaja kuwa kushindwa kutumia ipasavyo fedha za mgao wa kaunti kutoka kwa serikali kuu, hali ambayo amesema imewakosesha maendeleo na kuwaathiri moja kwa moja wananchi wa kaunti hiyo.

Akizungumza katika kongamano lililowaleta pamoja viongozi wa kijamii, kisiasa na kidini kutoka maeneo ya Nyali na Kisauni Mbogo amesema kuwa kila mwaka kaunti ya Mombasa hupokea takribani kima cha shilingi bilioni 17 kutoka kwa serikali kuu, fedha ambazo zinalenga kuboresha huduma za msingi kama afya, elimu, miundombinu, ajira kwa vijana na maendeleo ya kiuchumi.

Hata hivyo, amesema kuwa licha ya kiasi hicho kikubwa cha fedha, amesikitika  kutokana na kile alichokieleza kama matumizi duni, ukosefu wa mipango thabiti na utekelezaji hafifu wa miradi ya maendeleo.

“Ni jambo la kusikitisha sana kuona kaunti inapokea mabilioni ya fedha kila mwaka lakini wananchi bado wanahangaika kupata huduma za msingi. Vijana hawana ajira, barabara nyingi ziko katika hali mbaya, na sekta ya afya bado inakabiliwa na changamoto nyingi. Hili ni suala la uwajibikaji wa uongozi,” amesema Mbogo.

Kauli hii inajiri kufuatia ripoti ya mdhibiti wa bajeti wa serikali ambayo imemuorodhesha Gavana wa Mombasa kuwa miongoni mwa magavana waliotumia asilimia sifuri ya   migao ya fedha iliyotolewa na serikali kuu.

Mbogo amesema ripoti hiyo ni ishara tosha kwamba kuna changamoto kubwa katika usimamizi wa rasilimali za umma, akisisitiza kuwa fedha za wananchi hazipaswi kukaa bila kutumika ilhali mahitaji ya wananchi yanaendelea kuongezeka na ipo haja ya kuziba mianya ya ufisadi uliokithiri katika serikali ya kaunti ya Mombasa.

Ameongeza kuwa uongozi bora unapaswa kuongozwa na maono, mipango madhubuti na dhamira dhabiti ya kuhudumia wananchi, akisema kuwa kaunti ya Mombasa ina rasilimali na uwezo mkubwa wa kiuchumi endapo fedha zinazopatikana zitatumika kwa uwazi na ufanisi unaofaa zaidi. 

Wakati huohuo Mbogo amewataka viongozi wa kuweka maslahi ya wananchi mbele na kuepuka siasa zinazokwamisha maendeleo.

Kwa upande wao, viongozi wa kidini waliohudhuria kongamano hilo wakiongozwa na Patricia Ndioka wamesifu azma, dira na manifesto ya Ali Menza Mbogo, wakisema kuwa mtazamo wake wa uongozi una nafasi kubwa ya kuunganisha jamii ya Mombasa ambayo imekuwa ikikumbwa na migawanyiko ya kidini, kikabila na ya rangi na ukabila.

Viongozi  hao aidha wamesema kuwa ushirikiano kati ya viongozi wa kisiasa, kidini na kijamii ni muhimu katika kujenga mshikamano, amani na maendeleo endelevu.

“Tunahitaji viongozi wanaoweza kuunganisha watu wote bila kujali dini, kabila au rangi. Azma ya Ali Menza Mbogo inaonyesha nia ya dhati ya kuwaleta watu pamoja na kuijenga Mombasa kwa misingi ya umoja na maendeleo ya pamoja,” amesema mmoja wa viongozi wa kidini.

Viongozi hao wamewataka wananchi wa Mombasa kuwa makini wanapochagua viongozi wao, wakisisitiza umuhimu wa kuchagua uongozi unaowajibika, unaothamini matumizi bora ya fedha za umma na unaolenga kuboresha maisha ya wananchi kwa vitendo na si kwa maneno pekee.

Wamesema kuwa mustakabali wa kaunti hiyo unategemea maamuzi sahihi ya kisiasa yanayoweka mbele maslahi ya wananchi na maendeleo ya muda mrefu.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!