AFUENI KWA WAJAWAZITO KILIFI: SERIKALI YA KAUNTI NA SAFARICOM WAZINDUA ZAHANATI YA UZAZI YA SHILINGI MILIONI 300.
By Dayo Radio
Published on 18/12/2025 12:13
News

Ni afueni kubwa kwa wanawake wajawazito katika Kaunti ya Kilifi baada ya serikali ya kaunti hiyo, kwa ushirikiano na kampuni ya Safaricom, kuzindua zahanati ya kisasa ya uzazi yenye thamani ya shilingi milioni 300, hatua inayolenga kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto kote kauntini.

Akizungumza katika eneo la Bamba, eneobunge la Ganze, wakati wa kuweka jiwe la msingi la zahanati hiyo ya kujifungulia wanawake wajawazito chini ya mpango wa Uzazi Salama, Gavana wa Kaunti ya Kilifi, Gedion Mung’aro, amesema kuwa ujenzi wa zahanati mbalimbali za uzazi ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali ya kaunti wa kupunguza vifo vya kina mama wakati wa kujifungua na kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia wananchi kwa urahisi.

“Uzinduzi wa zahanati hizi za uzazi ni hatua muhimu katika kuhakikisha wanawake wajawazito wanapata huduma bora za afya karibu na walipo bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizi muhimu,” amesema Gavana Mung’aro.

Gavana huyo amesisitiza kuwa kwa muda mrefu wanawake wengi wajawazito wamekuwa wakikumbwa na changamoto za kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za kujifungua, hali ambayo imekuwa ikihatarisha maisha yao na watoto wao. Ameongeza kuwa serikali ya kaunti imechukua jukumu la kuwekeza pakubwa katika sekta ya afya ili kuondoa changamoto hizo na kuhakikisha kila mama mjamzito anajifungua katika mazingira salama na yenye huduma za kisasa.

“Tumewekeza pakubwa kuhakikisha zahanati hizi zina vifaa vya kisasa, dawa za kutosha pamoja na wahudumu wa afya wenye ujuzi, ili wakazi wa Kilifi wapate huduma bora na za uhakika,” amesema Mung’aro.

Aidha, Gavana Mung’aro ameeleza kuwa ushirikiano kati ya serikali ya kaunti na kampuni ya Safaricom ni mfano wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi unaolenga kuboresha maisha ya wananchi, hususan katika sekta nyeti kama afya. Amesema ushirikiano huo utawezesha ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya afya na kuongeza upatikanaji wa huduma kwa jamii za maeneo ya mashinani.

Wakati huo huo, gavana huyo ametetea mkataba mpya wa afya kati ya Kenya na Marekani, akisema kuwa mkataba huo utafaidi kwa kiwango kikubwa serikali za kaunti kwa kuongeza rasilimali, teknolojia na ujuzi katika sekta ya afya.

“Mkataba huu wa afya kati ya Kenya na Marekani utaimarisha sekta ya afya nchini, kuzijengea uwezo serikali za kaunti na hatimaye kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi,” amesema Gavana Mung’aro.

Amehitimisha kwa kutoa wito kwa wakazi wa Kilifi kushirikiana na serikali ya kaunti katika kulinda na kutumia ipasavyo vituo vya afya vinavyojengwa, akisema kuwa maendeleo ya kweli yanapatikana pale jamii inapochukua umiliki wa miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha yao.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!