Wazazi na jamii kwa katika eneobunge la Kisauni wameshauriwa kutumia njia mbadala za kutatua migogoro na kutoa suluhisho mwafaka kwa changamoto za ukosefu wa maadili miongoni mwa watoto, ili kuwasaidia kurejea na kukubalika upya.
Akizungumza katika kikao cha kuelimishajamiikuhusu namna ya kuwalea watotokatika maadilimema, mratibu wa mradi huo wa AMKENI WAKENYA kutoka chuo kikuu cha Nairobi Nayfeel Omar, amesema kuwa watoto wanaojikuta wakipelekwa kortini kutokana na makosa ya kimaadili hawapaswi kutengwa, bali ni vyema wapokelewe, waelekezwe na kupewa mwongozo unaofaa ili warejee katika mwenendo unaostahili.
Hata hivyo ameeleza kuwa malezi na ushirikiano wa wazazi pamoja na jamii kwa ujumla ni nguzo muhimu katika kumjenga mtoto kimaadili.
“Watoto wanaokosea kimaadili na hata kujikuta wakipelekwa kortini hawapaswi kutengwa au kuonekana kama waliopotea kabisa. Badala yake, wanahitaji kupokelewa na jamii, kupewa malezi, ushauri na mwongozo sahihi ili waweze kurejea katika mwenendo mwema. Malezi bora huanza nyumbani, lakini yanahitaji ushirikiano wa wazazi, viongozi na jamii kwa ujumla.”amesema Nayfeel.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Naibu Kamishna wa Kaunti ndogo ya Kisauni (DCC), Jamleck Mbuba, ambaye amesisitiza kuwa jamii ina jukumu kubwa katika kuwalea watoto na kuwajengea misingi imara ya maadili mema huku akiongeza kuwa idara ya usalama haitaruhusu mtu yeyote kuvunja sheria zilizowekwa na serikali.
“Tunawahimiza wazazi na jamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto, lakini hatutavumilia ukiukwaji wa sheria. Tuko tayari kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayekwenda kinyume na sheria,” amesema Mbuva.
Kikao hicho kililenga kuhamasisha mshikamano wa jamii, wazazi na vyombo vya usalama katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto za kimaadili miongoni mwa watoto na vijana katika eneobunge la Kisauni.
NA HARRISON KAZUNGU.