Aliyekuwa Mbunge wa Kisauni na Mwenyekiti wa Bodi ya Mradi wa Lamu Port–South Sudan–Ethiopia Transport (LAPSSET), Ali Menza Mbogo, ameendelea kuimarisha azma yake ya kuwania kiti cha ugavana wa Kaunti ya Mombasa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027 kwa kufanya misururu ya mikutano ya kisiasa na wakazi wa maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo.
Akihutubia mamia ya wafuasi wake katika mkutano wa kisiasa uliofanyika eneo la Bamburi siku ya Jumamosi, Mbogo alisisitiza dhamira yake ya kuongoza kwa kuzingatia maendeleo jumuishi na maslahi ya wananchi.
“Nimejitolea kuiongoza Mombasa kwa misingi ya maendeleo ya kiuchumi, uwezeshaji wa vijana na wanawake, na kulinda maslahi ya kila mkazi bila ubaguzi,” alisema Mbogo.

Alibainisha kuwa kaunti ya Mombasa ina fursa nyingi za kiuchumi ambazo bado hazijatumiwa ipasavyo, akisisitiza haja ya uongozi wenye maono.
“Mombasa ina uwezo mkubwa wa kiuchumi, lakini ni lazima tuwe na uongozi unaojali wananchi na unaofungua nafasi za ajira kwa vijana wetu,” aliongeza.
Mbogo alisema kampeni yake inalenga kuunganisha jamii zote na kujenga muungano mpana wa kisiasa unaolenga maendeleo ya kaunti.
“Hii si kampeni ya mtu mmoja, ni kampeni ya wananchi wa Mombasa. Nataka kujenga muungano wa kisiasa unaolenga maendeleo, mshikamano na ustawi wa wote,” alisema.

Aidha, aliwataka wakazi wa Mombasa kushiriki kikamilifu katika michakato ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
“Nawahimiza vijana, wanawake na wananchi wote kujitokeza, kushiriki kikamilifu katika siasa na kuhakikisha sauti zao zinasikika ili tuweze kushinda na kuleta mabadiliko chanya Mombasa,” alihitimisha Mbogo.
NA HARRISON KAZUNGU.